
Ama kweli kifo cha Mheshimiwa Amina Chifupa kimegusa wengi. Jana nimeshinda kwenye simu na neti kwenye e-mails naongea na watu kuhusu kifo chake. Kifo chake kimegusa wengi.
*********************************************************************
From ippmedia.com:
Wabunge kibao waangua vilio
2007-06-27
Na Emmanuel Lengwa, Mikocheni
Kama kuna siku ambayo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limegubikwa na simanzi, basi ni leo asubuhi wakati Spika, Samweli Sitta alipowatangazia wabunge kwamba mwenzao, mheshimiwa Amina Chifupa, amefariki dunia.
Baada ya taarifa hiyo, wabunge wengi walishindwa kujizuia na kuanza kuangua kilio waziwazi. Mbunge Jenista Mhagama, Aziza Sleyum, Martha Mlaka na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Margareth Sitta ni miongoni mwa wengi waliokuwa wakibubujikwa machozi waziwazi na kuwalazimu wabunge wengine kujipa ushujaa wa kuwafariji muda wote. Vilio hivyo na simanzi vilishika kasi zaidi wakati wabunge wote walipotulia vitini ili kumsikiliza Spika wa Bunge, Mhe. Sitta wakati akiendelea kueleza utaratibu unaofuata.
Kadhalika hapa Jijini Dar, nyumbani kwao marehemu Amina, vilio vilitawala huku ndugu na jamaa wakiwa hawaamini kama kweli mpendwa wao amewatoka. Alasiri ilipotinga nyumbani kwa baba wa marehemu, Brigedia mstaafu Chifupa, Mikocheni Jijini leo asubuhi imemkuta aliyekuwa mume wa marehemu pamoja na na familia yake, wakiwa katika majonzi makubwa.
Akizungumza na Alasiri, Bw. Mohamed Mpakanjia, amesema mazishi ya aliyekuwa mkewe yanatarajiwa kufanyika kesho huko wilayani Njombe. ``Tutaondoka kesho kwenda Njombe kwa mazishi? leo tunatoa fursa kwa ndugu, jamaa na marafiki na wananchi wa waliopo Jijini Dar ili kuweza kumuaga kabla ya kumsafirisha,`` akasema Bw. Mpakanjia.
Bw. Mpakanjia amesema ikiwa ratiba itakwenda kama ilivyopangwa, baada ya wabunge kutoa heshima za mwisho, mwili wa marehemu utaondoka kwa ndege kuelekea Njombe ambako utazikwa kesho,? akasema. Kabla ya kifo chake, Mheshimiwa Chifupa anakumbukwa jinsi alivyokuwa akitoa hoja kadhaa nzito nzito bungeni.
Marehemu alikuwa akiwashangaza wengi kutokana na ujasiri wake wa kuibua mambo mazito kama yale ya kujitolea kuongoza mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya waziwazi, jambo ambalo wazoefu wengi wamekuwa hawaonekani kulifanya.
Pia alikuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya vijana, kukemea rushwa na kupigania haki za wanawake.
Historia ya mbunge huyo aliyekuwa miongoni mwa waheshimiwa wenye umri mdogo zaidi katika bunge la sasa inaonyesha kuwa amepata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Ushindi ya Jijini, kisha akajiunga na shule ya sekondari ya Kisutu. Alipomaliza kidato cha nne, Amina Chifupa alijiunga kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Makongo kabla ya kuhitimu na kwenda kujiunga katika Chuo cha Uandishi wa Habari cha Royal College cha Jijini Dar es Salaam. Inaonyesha historia yake kuwa tangu akiwa shuleni, marehemu Amina alishaanza kazi ya utangazaji wa redio. Mwaka 2005, Amina Chifupa alitwaa ubunge baada ya kufanya vyema katika uchaguzi mkuu kupitia tiketi ya viti maalum (Vijana-CCM).
Hadi anafariki dunia jana usiku, marehemu Amina Chifupa alikuwa na umri wa miaka 27.