
Jeneza lenye mwili wa Marehemu Amina Chifupa
From ippmedia.com
Bunge laahirishwa...mwili kuagwa leo
2007-06-27
Na Usu-Emma Sindila, Dodoma
Kifo cha Mbunge wa Viti Maalum-CCM, Mheshimiwa Amina Chifupa kimelifanya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuahirisha shughuli zake ili kujipa muda wa kumlilia mwenzao, Mheshimiwa Amina Chifupa aliyefariki usiku wa kuamkia leo.
Spika wa Bunge, Mhe. Samweli Sitta amesema shughuli za Bunge zitaendelea tena kesho asubuhi saa tatu. Hata hivyo amesema wabunge kadhaa wameteuliwa kuja Jijini Dar es Salaam kuungana na ndugu wa marehemu kuomboleza na kushiriki shughuli nyingine za msiba huo mzito.
Awali ilikuwa imetangazwa kwamba mwili wa marehemu ungepelekwa Dodoma kuagwa na kisha kusafirishwa kwenda Njombe kwa maziko.
Spika amewataja watakaoongoza msafara huo wa wabunge kwa ajili ya kuuaga mwili na kisha kesho kushiriki maziko kule kijijini Lupembe wilayani Njombe kuwa ni pamoja na yeye mwenyewe, kiongozi wa upinzani bungeni, Mhe. Hamad Rashid Mohamed, wabunge wote wa Dar es Salaam, wabunge wote wa Iringa na Mbunge Anne Kilango aliyekuwa mlezi wa marehemu.
Amesema watakaowakilisha Serikali katika msiba huo ni Waziri wa Usalama wa Raia, Bw. Bakari Mwapachu. Amesema marehemu atazikwa kesho katika kijiji cha Lupembe wilayani Njombe kule Iringa, alasiri. Kwa mujibu wa Spika Sitta taarifa marehemu alifariki usiku wa kuamkia leo katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo Jijini Dar.